Monday, June 11, 2007

CCM itajuta ikikubali mseto zanzibar

CCM itajuta ikikubali mseto Zanzibar

Na Ali Mwinyi Msuko

Zumari likipulizwa Zanzibar wahemkwao walio Bara huu ni msemo maarufu uliokuwa ukitumiwa Zanzibar hapo kale, lakini badala ya kuhemkwa walio Bara sasa zama hizi za Utandawazi ni zamu ya wale wa Mtendani Unguja, sehemu ambako yako Makao Makuu ya Chama cha CUF.

Watu wa Mtendani hawana tofauti na wananchi wa Taifa la “ Kusadikika” Wasadikika kila kitu walichoambiwa na wakuu wao waliamini, hakuna anayebisha wala kuhoji hiyo ndiyo sifa kubwa ya wasadikika. Katika kitabu kilichotungwa na marehemu Shabaan Robert cha Kusadikika ukikisoma kwa makini ni dhahiri kuwa kinachoelezwa hivi sasa wanasiasa wa kambi ya upinzani Zanzibar ni mambo ya kusadikika.

Seif Shariff naposhindwa Uchaguzi huwa hakosi visingizio. Visingizio vyake vikubwa ni kuibiwa kura zake, kuzua uongo kuwa Uchaguzi haukwa wa haki na huru. Na wakati mwengine kudai kuwa Tume ya Uchaguzi imependelea Chama Tawala. Kila unapomalizika Uchaguzi yeye hubeba bango la kuibiwa kura, Tume ya Uchaguzi kupendelea chama tawala na kuwa Uchaguzi haukuwa wa haki na huru. Atafanya kila aina ya vitimbi almuradi nchi iingie katika misukosuko ili yeye apate manufaa.

Baada ya kutangazwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2005 Zanzibar, CCM iliinuka kidedea kuwa mshindi kwa kushinda Majimbo 31 dhidi ya Majimbo19 iliyopata Chama Cha Upinzani cha CUF. Na katika kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar katika Uchaguzi huo, Mgombea wa CCM ,Amani Abeid Karume alishinda kwa kupata kura 239,882 sawa na asilimia 53.2% akifuatiwa na Mgombea wa CUF Seif Shariff Hamad aliyepata kura 207,733 sawa na asilimia 46.1%, wengine ni bwana Haji Mussa Haji Kitole wa Jahazi Assilia alipata kura 2110 sawa na asilimia 0.5%, bwana Ali Abdulla Ali wa chama cha DP alipata kura 509 sawa na asilimia 0.1%, bwana Simai Abdulrahman Abdulla wa NRA alipata kura 449 sawa na asilimia 0.1%, na wa mwisho bibi Maryam Ahmed Omar wa Chama Cha SAU alipata kura 335 sawa na asilimia 0.1%.

Kwa matokeo hayo inaonesha dhahiri kuwa Rais Amani Abeid Karume amepata ushindi usioshaka dhidi ya wapinzani wake watano. Kwani ushindi wake umepindukia asilimia 50% ya kura halali, Karume amepata ushindi wa Asilimia 53.2% na ndio maana tunasema ameshinda kwa kishindo.

Kwa kuwa Rais Karume ameshinda kiti cha Urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa 2005 na Chama chake kimeshinda Majimbo 31 kati ya Majimbo 50 ya viti vya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ikiwa sawa na asilimia 62.% hapo hapakuwa na utata wa kumzuwia Rais Karume kuunda Serikali, tena Serikali ya CCM ambayo itakuwa na wajibu wa kutekeleza Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa 2005 – 2010, Ilani ambayo ilinadiwa kwa wapiga kura katika kampeni za Uchaguzi huo ikiwa kama ahadi za CCM nini kitawafanyia wananchi pindipo wakiichagua. Baada ya wananchi kuridhika na na ahadi za CCM. Waliamua kwa ridhaa yao kukipa kura zao kwa kukichagua kuongoza Dola kwa kipindi cha miaka mitano (5) ijayo.

Kwa mujibu wa maelezo hayo Serikali iliyopo madarakani sasa hapa Zanzibar, ni Serikali halali na ni ya Kidemokrasia iliyoundwa kwa mujibu wa Katiba na sheria zilizowekwa, kwa sababu imepata ridhaa ya wananchi walio wengi wa Zanzibar.

Kanuni ya Demokrasia inasema Mgombea au Chama chochote kilichopata kura na viti vingi kuliko vyengine huwa ndio kimechaguliwa na kimepewa ridhaa na wananchi ya kutawala. Hili ndilo lililofanyika Zanzibar baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2005. Rais Karume kashinda Urais wa Zanzibar kupitia Chama chake kilichomteua kugombea kiti hicho, na Chama chake CCM kimeshinda viti vya Uwakilishi vya Majimbo ya Zanzibar kwa zaidi ya asilimia 50%. Hili halina ubishi wala halitaki tochi.

Kwanini tunasema kuwa Zanzibar haina mazingira ya kuundwa Serikali ya Mseto.? Hapa nataka niwafahamishe baadhi ya wale wasioelewa na hususan jamaa zangu wa Taifa la Kusadikika ambao kila uchao wanasadiki kila wanachoambiwa na Yuda Iskarioti,

Nchi yoyote katika ikitaka kuunda Serikali ya Kidemokrasia, kwanza lazima iwe na Katiba ambayo itafafanua jinsi ya nchi husika itakavyoingia katika Utawala utakapewa ridhaa na wananchi wenyewe. Zanzibar wakati tulipoamua kuingia katika mfumo wa Siasa wa vyama vingi mwaka 1992 mwezi Julai tulikuwa na Katiba yetu. Haidhuru Katiba hiyo ilikuwa ya mfumo wa Chama kimoja lakini ilifanyiwa marekebisho ili iruhusu mfumo wa vyama vingi vya Siasa. Na sheria zetu hasa za Uchaguzi pamoja na Kanuni nyingi ilibidi zirekebishwe ili ziende sawiya na mazingira ya mfumo uliokuwepo.

Pamoja na kufanya mabadiliko ya Katiba na Sheria, Katiba yetu iliweka wazi utaratibu wa kisheria wa namna mfumo wetu wa Uchaguzi utakavyokuwa. Kwa hapa kwetu tulikubaliana kufuata mfumo wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Madola. Mfumo ambao unampa nafasi ya kuchukuwa kila kitu anaeshinda . Mfumo huu utaratibu wake Mgombea Kiti cha Urais si lazima kupata asilimia fulani ya kura, isipokuwa Mgombea atakaeongoza kwa kura ndiye atakaetangazwa kuwa mshindi.
Na kwa upande wa viti vya Wabunge/Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Chama kitakachopata viti zaidi ya nusu ndicho kitakachotoa Waziri Kiongozi (Waziri Mkuu ) na kupewa nafasi ya kuunda Serikali. Pindipo ikitokea kuwa hakuna Chama kilichopata viti zaidi ya nusu, hapo ndipo yatakapotokea mazingira ya Vyama vitakavyokubaliana kwa masharti watakayowekeana wataunganisha viti vyao ili wapate kuunda Serikali, hii itakuwa ndio Serikali ya Mseto. Vyama vinavyokubaliana kuunda Serikali ya Mseto lazima Sera zake ziwe zinalingana au Chama chenye viti kidogo kikubali kutekeleza sera za Chama kilichokuwa na viti vingi.

Pamoja na malengo na madhumuni mengine ya chama chochote cha siasa, lakini lengo kuu ni kushinda Uchaguzi ili kipate fursa ya kuunda Serikali.
Kwa mfano katika Chama Cha Mapinduzi hili ni dhumuni la Kikatiba kwani limeainishwa katika Katiba yake Toleo la Mei 2005 “Kushinda katika Uchaguzi wa Srikali Kuu na Serkali za Mitaa Tanzania Bara na Zanzibar ili kuunda na kushika Srekali Kuu na Serikali za Mitaa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande mmoja na Zanzibar kwa upande mwengine”inasomeka sehemu ya kwanza Ibara ya 5(1) ya Katiba hiyo.

Kwa hivyo naamini kuwa vyama vyote vya siasa vilivyoundwa moja kati ya malengo yake ni kushinda Uchaguzi ili viweze kuunda Serikali. Kwa sababu ya kutaka kulifikia lengo hilo ndio maana vyama vya siasa vinasimamisha wagombea wa nafasi mbali mbali katika Uchaguzi Mkuu na kushiriki katika kuwafanyia kampeni wagombea wao ili washinde. Lakini vile vile Chama cha Siasa kinatakiwa kuelewa kuwa, kunako ushindani kunakuwa na matokeo mawili, kushinda na kushindwa.

Hivyo chama cha Siasa kinapoingia kwenye ushindani lazima kijiandae kupokea matokeo yote mawili, kwani chama cha Siasa kitakaposhikilia kuwa lazima kishinde, Chama hicho kitakua si cha Kidemokrasia. Tena ni vyema wananchi wakakiepuka, kwani kinaweza kusababisha maafa makubwa katika nchi.

Kutokana na maelezo ya hapo juu, kwa mtu mwenye akili anafahamu kuwa Chama Cha Mapinduzi kushinda Uchaguzi na kuunda Serikali, ni jukumu lake la Kikatiba, na inatekeleza katiba yake iliyoiunda na kuipitisha katika Kikao chake cha Mkutano Muu wa Taifa. Sasa tujiulize sisi watu wenye akili timamu. CCM imeshinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 kwa mgombea wake wa kiti cha Urais wa Zanzibar kupata kura nyingi zaidi kuliko wagombea wa vyama vyengine, na kushinda zaidi ya asilimia 50% ya viti vya Majimbo, bado haina haki ya kuunda Serikali yake peke yake? Au kwa kuwa kuna mgombea wa chama fulani naye kapata kura nyingi si haba, kuwa inatosha kuwa kipimo cha kuilazimisha CCM kuunda Serikali ya Mseto ?.
Chama Cha Mapinduzi kikifanya hivyo, kwanza kitakuwa kinaikiuka Katiba yake, na pili kitakuwa kinaipinga Katiba ya nchi na Sheria za Uchaguzi. Makubaliano yetu Chama kilichoshindwa madam kimepata Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waunde Kambi ya Upinzani ndani ya Baraza. Au Chama cha CUF hakiridhiki na nafasi ya upinzani kiliyoipata?

Kama chama Cha CUF hakiridhiki na nafasi ya kuwa ni Chama cha Upinzani ndani ya Baraza la Wawakilishi basi hakuna haja ya kuwa na Uchaguzi wa vyama vingi nchini. Na hata huo Mfumo wa vyama vingi vya Siasa hauna haja ya kuwepo. Sababu ya kuwepo kwa mfumo huu ni kukuza Demokrasia, kuwa na Utawala bora unauzingatia Sheria, vile vile kuwa na Wawakilishi wa upinzani ndani ya Baraza la Kutunga Sheria watakaoweza kuihoji na kuikosoa Serikali pindipo inapofanya vibaya, lakini Serikali inapofanya vizuri, hawana budi kuisifu na kuipongeza kwa nguvu zote.

Tatizo la Zanzibar linatokana na viongozi wa Chama Cha CUF kwanza kuyakataa matokeo na kutokukubali kuwa wameshindwa katika Uchaguzi. Jambo hili lilijitokeza tangu Uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi 1995 ambapo Mgombea wa CCM Dr. Salmin Amour (Komandoo) alimshinda Mgombea wa CUF Seif Sharif Hamad. Na katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 Mgombea wa CCM Rais Karume, alimshinda vibaya Seif Shariff. Lakini mara zote mbili Seif Sharif na Chama chake cha CUF waliyakataa matokeo.

Katika Uchaguzi wa 1995 CCM ilipata viti vingi zaidi kuliko CUF hivyo ikaunda Serikali. Haidhuru matokeo hayo hayakutafautiani na ya 2005 kwani CUF ilishinda viti vyote vya Majimbo ya Pemba na CCM ikashinda Majimbo yote ya Unguja. Lakini Dr. Salmin Amour aliunda Serikali ya CCM na CUF ikawa ni Chama cha Upinzani katika Baraza la Wawakilishi. Kwa kuwa Dr. Salmini Amour alishinda kwa asilimia ndogo ya kura 50.2% na Seif Shariff alipata asilimia 49.8% hoja ya Seif Sharif ya kukataa matokeo ilipewa nguvu akapata kuungwa mkono na Afisi za Ubalozi wa Mataifa ya nje na baadhi ya Jumuiya za Kimataifa.

Lakini katika Uchaguzi wa mwaka 2000 Rais Karume alishinda kwa asilimia kubwa zaidi na Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi huo kikapata viti vingi zaidi, kwani kilishinda Majimbo yote ya Unguja na kupata viti katika Majimbo matano ya Pemba . Matokeo hayo yakampa fursa Karume kuunda Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Kama kawaida yake Seif Shariff aliyakataa matokeo hayo, na kuwataka Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CUF kuligomea Baraza. Kulikuwa na sababu gani kuwaziwia Wawakilishi wa chama chake kuingia katika Baraza. Au ndiyo ile
Kauli mbiu yao ya “Akipata Seif tumepata sote na akikosa tumekosa sote.?Kwa kuwa Mashirika mengi ya Kimataifa pamoja na nchi wahisani walileta wajumbe wao kwa madhumuni ya kuangali mwenendo mzima wa Uchaguzi huo. Waangalizi wa Kimataifa waliridhika na mwenendo wa Uchaguzi na waliyakubali matokeo yake, hapo ndipo Seif Sharif alipokosa hoja na sababu ya kuyakataa matokeo hayo.

Pamoja na kuwazuia Wawakilishi wa Chama chake kushiriki katika vikao vya Baraza, lakini safari hii amekuja na mpango mpya wa kuhakikisha nchi haitawaliki. Alijuwa kuwa Uchaguzi hauwezi kurudiwa, wala hakuna nafasi ya Serikali ya Mseto. Aliandaa mazingira ya fujo kwa kuwahamasisha wafuasi wa Chama chake kufanya fujo na vurugu kwa kufanya Maandamano ambayo alijua kuwa Vyombo vya Dola havitayaruhusu, lengo lake yatokee mapambano kati ya wafuasi wake na Vyombo vya Dola.

Mpango wake ulifanikiwa kwani Januari 26 na 27 mwaka 2001, wafuasi wa CUF walifanya Maandamano haramu huko Pemba hasa katika Miji ya Wete, Chake Chake, Mkoani na Michewerni. La ajabu maandamano hayo hayakuwa na kituo cha kuanzia wala cha kumalizia. Pia hayakuwa na Mgeni Rasmi wa kuyapoke. Siku hiyo, wafuasi wa CUF walianza kwa kuelekea katika Vituo vya Polisi. Mjini Wete, walimchinja askari wa Jeshi la Polisi kama kuku kwa kutenganisha kichwa mbali na mwili mbali. Baadae wakaelekea kituo cha Polisi kwa nia ya kukiteka. Yaliyotokea Seif alikuwa anyajua kabla, na aliyapanga kwa makusudi. Lakini kwake yeye kufa watu hamsini au mia moja si kitu almuradi anayoyataka yawe.

Kubwa analolitaka ni maslahi yake binafsi wala sio ya wanachama wa chama chake au wananchi kwa ujumla. Kubwa zaidi alikuwa anatengeneza siasa yake na ya chama chake, kwani alikuwa anajua kama angekubali matokeo ya Uchaguzi na kukaa kimya akisubiri Uchaguzi mwengine ajaribu bahati yake, mambo yake yasingemnyookea. Angelikosa maslahi yake na jukwaa la kisiasa, na baya zaidi kwake angekimbiwa na wafuasi wake. Kwani alikwishawaahidi kupata ushindi na hatimae kuunda Serikali.

Baada ya matokeo hayo kama kawaida Serikali ilibidi kuwasaka wahusika wa maandalizi ya Maandamano hayo haramu. Hapo Seif Shariff na chama chake mtego wao ukawa tayari umenasa. Nakumbuka tulipokuwa wadogo wakati tukiweka mitego ya ndege maporini, mtu akikuta mtego wake umenasa anafurahi sana, kwani lengo lake limekuwa. Lengo kubwa la Seif yeye kutaka ukubwa wa kutawala nchi na zaidi kulinufaisha tumbo lake pengine yeye ni mmoja kati ya wanasiasa wa sera ya matumbo


Kadhia hii ilikuwa nzito katika nchi yetu, kwani mambo mawili haya hayakuwa ya mchezo hata kidogo, Wapinzani kususia Baraza, kupotea kwa roho za watu na Tanzania kuzalisha wakimbizi. Nipo mgogoro uliokuwa ukipigiwa mbiu na CUF, ukaonekana kuwa upo, haidhuru mgogoro wenyewe ni wa kutengenezwa na chama cha CUF kwa maslahi ya viongozi wake wachache.

Kwa kuwa Chama Cha Mapinduzi ndicho kilichokuwa na dhamana ya nchi, kililazimika kutafuta namna ya kurudisha hali iwe ya kawaida katika nchi. Busara ikatumika kwa viongozi wa CCM kukaa kwenye meza moja na viongozi wa CUF kwa mazungumzo. Hapo ndipo ulipopatikana Mwafaka wa pili kati ya Vyama vya CCM na CUF. Katika kuutengeza Mwafaka huo Seif na chama chake walidai mambo lukuki, mengine hata mtoto mdogo hawezi kuyadai kwa mzazi wake. Mfano CUF walidai kuwa:-
§ Uchaguzi wa Zanziba urudiwe kwa sababu haukuwa wa haki na huru.
§ Aidha iundwe Serikali ya Mseto na kutaka Waziri Kiongozi wa SMZ atoke katika chama chao.
§ Pia wapewe nafasi za Uwaziri katika badhi ya Wizara za SMZ
§ Wapewe nafasi za Ukuu wa Mkoa na Wiliya katika baadhi ya Mikoa.
§ Viongozi wa kisiasa waliostaafu watambuliwe kisheria na kupewa haki zao.
§ Wananchi walioathirika katika harakati za kisiasa kwa kufukuzwa kazini, kubomolewa majumba yao, na wahanga wa tukio la tarehe 27, Januari 2001 walipwe fidia nk.

Kwa kuwa mambo mengi waliyoyataka yalikuwa hayawezikani lakini busara ikatumika kwa kupatiwa baadhi ya mambo. Lakini jambo la msingi iliundwa Tume ya Pamoja kati ya CCM na CUF na kuteuliwa Makamishna kutoka vyama hivyo kwa madhumuni ya kusimamia Mwafaka huo. Baada ya kusainiwa Mwafaka na baadhi ya mambo yaliokubaliwa yalianza kutekelezwa. Jambo lakwanza kabisa lilikuwa suala la Seif Shariff, kulipwa mafao yake na kutambuliwa kama

Waziri Kiongozi Mstaafu, hali ya kuwa hakupaswa kulipwa mafao hao kwani alifukuzwa katika Wadhifa huo kutokana na kwenda kinyume na maadili ya kazi yake. Aidha, baadhi ya wachanjagizi wake kuula kwa kupewa nafasi za Makamishna wa Tume ya Muafaka iliyojulikana kwa jina la Tume ya Pamoja ya Usimamizi wa Mwafaka (PRST). Baada Seif na wenzake walitulia. Kwani walilokuwa wanalitaka tayari wamekwisha kulipata. Zanzibar ikawa shuwari, hakuna tena kauli za kuhubiri vita, shari , fujo wala umwagaji wa damu.

Kwa upande wa wakimbizi waliokimbilia Shimoni nchini Kenye nao wakarejea. Isipokuwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CUF hawakuweza kurejea tena Barazani kwa sababu kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Baraza walikuwa si Wajumbe tena wa Baraza kwani walikwisha kufukuzwa. Katika hili Chama Cha Mapinduzi lazima kipewe pongezi kwa ujasiri uliouonesha katika kutekeleza makubaliano ya Mwafaka huu. Kwa sababu makubaliano mengine yalikuwa magumu kwa Chama Cha Mapinduzi, na mengine yalihitaji mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar. Hata hivyo CCM na Serikali yake ikapiga moyo konde na kuyatekeleza, na pale ilipobidi kurekebishwa vipengele vya Katiba basi vilirekebishwa. Jamii ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla, walishuhudia Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakifanya mabadiliko ya Ibara ya Nane na Tisa ya Katiba ya Zanzibar.

Moja katika suala zito lililotekelezwa ni kuiunda upya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na kuwashirikisha wajumbe wawili (2) kutoka chama cha upinzani. Aidha, jamii ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla, tulishuhudia Nassor Khamis na Ussi Khamis Haji (CUF), wakiteuliwa kuwa Wajumbe wa ZEC. Jukumu la kwanza la Tume hii mpya lilikuwa ni kusimamia Uchaguzi Mdogo wa Majimbo 17 ya Pemba uliofanyika mwaka 2003, Uchaguzi ambao ulitawaliwa na vituko ambavyo havitasahaulika katika masikio ya Wazanzibari.

Tangu kuanzia hatua ya uandikishaji wake hadi upigaji kura. Vituko vilandaliwa na Chama Cha Wananchi (CUF) kwa makusudi ili kuhakikisha wajumbe wao wa Baraza la Wawakilishi waliofukuzwa wanarudi tena Barazani.

Wakati wa kuajiri Maafisa na Watumishi wa Tume, walijipanga ili kuhakikisha nafasi zote zinashikiliwa na wafuasi wa chama chao. Ili kuweza kufanikisha azma yao hiyo, Wana CUF pamoja na mambo mengine, waliandaa mambo kadhaa ya shari ikiwa ni pamoja na kauli mbiu inayosema “Asie Husika Haandikishi”. Lengo kuu ni kuhamasisha wafuasi wao kumpinga mtu yeyote mwenye asili ya Unguja au Tanzania Bara ata akiwa na haki ya kuandikishwa kuwa mpiga kura basi asipate nafasi ya kujiandikisha.

Kweli waliitumia nafasi hii kwa kuwapinga wale wote waliokuwa na Asili ya Unguja na Tanzania Bara kwa kudhani tu kuwa walikuwa na msimamo wa Chama Cha Mapinduzi. Aidha, waliwekewa mkakati maalum askari wa aina yoyote pamoja na familia zao kutoandikishwa kuwa wapiga kura. Hapa ilijengwa imani kwa wana CUF kuwa Serikali ya SMZ imepeleka askari wa vikosi vyake eti kwa nia ya kupandikiza wapiga kura, jambo ambalo halikufanyika kabisa.

Wakati wa zoezi la uandikishaji likiendelea wananchi wenye asili ya Unguja na Tanzania Bara walipingwa iliwasijiandikishe kuwa wapiga kura hata kama Sheria ya Ukaazi inawaruhusu. Maafisa waandikishaji wapiga kura katika vituoni walikuwa wakiwasikiliza wakala wa Chama Cha CUF kwa lolote walilosema. Wakipinga mtu asiandikishwe hata kama anayo haki ya kujiandikisha basi haandikwi, na atakaesema aandikwe hata kama hana haki ya kuandikishwa basi ataandikwa. Na yule atakaejidai ujabari wa kudai haki yake atapokea vitisho vya kuhatarishiwa maisha.

Uchaguzi huu mdogo ulikuwa ulete tena maafa, kwani wana CCM nao walikuwa tayari kwa lolote ikiwa ni pamoja na kuwakabili wana CUF, lakini wahakikishe haki yao ya msingi na kikatiba ya kujiandikisha hawaipotezi. Kwa busara za viongozi wa CCM, waliwatuliza wanachama wao na hasa kwa kuzingatia Uchaguzi huo hata kama CCM haikupata kiti hata kimoja, usingeipunguzia sifa za kuendelea kushika hatamu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ulikuwa ni Uchaguzi wa kutekeleza Mwafaka tu.

Katika Uchaguzi huo mdogo wa majimbo 17 ya Pemba kulitokea matukio mengi makubwa na kushangaza mno na kutosahaulika katika jamii ya Wazanzibari. Miongoni mwa hayo ni lile la kupigia kura Maruhani. Ilikuwaje? Wakati Tume ya Uchaguzi ilipofanya uteuzi, Wagombea sita wa chama cha CUF waliwekewa pingamizi na chama cha NCCR Mageuzi, baada ya kuonekana kuwa kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi za Zanzibar wagombea hao hawawezi kugombea ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, waliondolewa katika orodha ya wagombea.

La ajabu lililotokea siku ya upigaji kura, pamoja na kuwa baadhi ya vyama vya upinzani vilisimamisha wagombea wao katika Majimbo hayo sita, lakini chama cha CUF kiliwashawishi wapiga kura watokanao na chama hicho, kutomchagua mgombea hata mmoja wa chama chochote kati ya hivyo na hivyo wengi wa wananchi wa majimbo hayo waliziharibu kura zao na kudai . Matokeo yake ikawa kura zilizoharibika ni nyigi zaidi kuliko zilizo amua kuwachagua wagombea wengine, wenyewe wakaziita kura za Maruhani. Hatimae Chama Cha Mapinduzi kikashinda viti sita vya Uwakilishi kiulaini katika Uchaguzi huo.

Hapa jambo la kujiuliza, hivi ni kweli katika kisiwa cha Pemba asipowekwa mgombea wa CUF katika Uchaguzi wanachama wa CUF hawatapiga kura? Au wataamua kura kuziharibu kwa maksudi? Hili ni tatizo kubwa hasa ukizingatia katika karne hii ya 21, karne ya Sayansi na Teknolojia, wananchi wanaodai haki na uhuru wa kuchagua viongozi wanaowataka wenyewe kufanya kitendo cha kijinga kama hicho.

Inadhihirika wazi kuwa kwa wanachama wa CUF wa Pemba ambao ndio wengi kuliko wanachama wa chama chengine chochote hawataki chama chengine cha upinzani isipikuwa CUF. Na nadhani ndipo pale Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete aliposema kuwa. Pemba kuna tatizo la kisiasa. Wananchi wa Pemba wanatakiwa kuelimishwa na kufahamishwa nini maana ya Demokrasia ya vyama vingi. Na nini haki ya mpiga kura katika uchaguzi wa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Seif Shariff na chama chake cha CUF wameliapandikiza tatizo la kisiasa miongoni mwa wananchi wa kisiwa cha Pemba hadi imefikia hali ya kuwa hasikilizwi mtu yeyote isipokuwa Seif Shariff, wala hakisikilizwi chama chochote isipokuwa CUF. Hata kitokee chama chenye sera nzuri namna gani wao hawakisikilizi, watakifumbia macho na kukizibia masikio, almuradi wao na Seif na CUF, atakalosema Seif ndio hilo hilo hata kama litakuwa na madhara kiasi gani, kwani bwana kasema!

Seif amewafanya wanachama wa chama chake hasa wa Pemba wasiitii Serkali yoyote ilioko madarakani isipokuwa Serikali ya CUF, na wasimtii kiongozi yeyote aliyekuweko madarakani isipokuwa Maalim Seif. Tunapenda kuwambia wana CUF hasa wa Pemba kuwa hili ni tatizo!

Seifaf Sharifu ana mradhi ya ukuwa, kwa hapa Zanzibar alikwishawahi kushi nafasi kubwa sana ya uongozi wan chi, alikuwa Waziri Kiongozi wa SMZ kuanzi Januari 1984 hadi mwishoni mwa mwaka 1988. Kwa tabia yake Seif kwakuwa hakupenda kumuona mtu mwengine akiwa juu yake, na nfasi ya juu ya uongozi kwa hapa Zanzibar ukiacha hiyo aliyokuwa nayo yeye wakati ule ni nafasi ya Urais wa Zanzibar.

Kwa hivyo Seif akaanza kufanya juhudi ya kuusaka Urais wa Zanzibar kwa uvumba na udi. Tangu akiwa ndani ya CCM wakati wa mfumo wa Chama kimoja kwa kupambana na Marehemu Mze Idriss Abdulwakil ndani ya Halmashauri Kuu ya Taifa mwaka 19985 wakati wa kutafuta mgombea Urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.

Tabia yake ya kutokukubali kushindwa ilianza kjitokeza hapo. Kwani Seif alishindwa na Marehemu Mzee Idriss nani ya Kikao cah Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa kura saba tu, lakini aliyakataa matokeo, nakuanza visingizio kuwa ameibiwa kura zake. Alipotoka hapo aliyoyafanya sote tumeyaona na hatimae alifukuzwa Uwaziri Kiongozi na baadae kwenye CCM yenyewe.

Kama tulivyo tangulia kuandika hapuko nyuma katika waraka huu kuwa Seif Shariff hakubali kushindwa, na anaposhindwa atajaribu kutafuta kila kisingizio. Katika Uchaguzi Mkuu wa 2005 Seif ameshindwa tena, na kwakuwa nchi Wahisani na Mashirika ya Kimataifa mengi tu walileta waangali wao. Katika Taarifa za Taasisi zilizokuja kuangalia Uchaguzi huu zote zimeeleza kuwa Uchagu Mkuu wa Zanzibar ulikuwa huru na wa haki, na uliendeshwa kwa uwazi zaidi. Kwa mfano Taasisi ya National Democratic Institute for International Affairs (NDI) ambayo Makao Makuu yake yako Washington DC nchini Marekani.

Katika taarifa yao ya mwisho waliyoitoa Novemba 28,2005, kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Octoba 30,2005 walikubali kuwa Uchaguzi wa mwaka huu umeendeshwa vizuri kuliko chaguzi zilizopita. Kwa kuwa Seif ulalamishi wake alikuwa akitegemea sana Taarifa za Waangalizi wa Uchaguzi wawe wa ndani au wa nje, ikiwa waangalizi hao walitoa kasoro ndogo tu, basi yeye atairemba, atakuza na kuipamba mpaka ionekane kuwa Uchaguzi wote hauna maana ili apate kudai Uchaguzi urudiwe.

Baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Octoba 30,2005, Seif Sharifu alipigwa na butwaa asijue la kufanya, akawa hana la kusema. Kwani alikuwa anajua fika kwamba atashindwa, lakini safari hii hakuna Afisi ya Ubalozi wa nchi za nje, wala Mashirika ya kimataifa yaliyotilia shaka matokeo ya Uchaguzi huu. Jambo ambalo Seif na chama chake lilizidi kuwatia bumbuwazi.

Hata hivyo hakuwacha kutoa visingizio vyake kuwa Uchaguzi umevurugwa na yeye ndiye mshindi lakini kafanyiwa mbarange. Inasemekana hata katika kikao cha Chama chao cha kwanza baada ya matokeo hayo hawakuwa na uamuzi wa nini wafanye. Kwa muda mrefu alibaki kulalama tu kwa kupiga kele ambazo hazikuwa na msikilizaji., kwani “Kelele za mlango hazimuasi mwenye nyumba kulala”.

Kwa kuwa matokeo ya Uchaguz yaliigawa Zanzibar kivyama, Majimbo ya Pemba yote yalichukuliwa na CUF na yale ya Unguja yote yakachukuliwa na CCM isipokuwa Jimbo moja tu, la Mji Mkongwe. Na kwa upande wa kura za Urais Seif alipata kura nyingi Pemba kuliko Karume ambaye alipata kura nyingi zaidi kuliko Seif Shariff katika kisiwa cah Unguja,

Na tukizingatia kuwa Unguja kuna Majimbo mengi zaidi na wapiga kura wengi zaidi kuliko Pemba. Jambo ambalo lilipelekea Rais Karume kuunda Serkali ambayo ina Mawaziri wengi kutoka kisiwa cha Unguja. Hili limetokea kwa sababu kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar Mawaziri huwa wanatokaba na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Majimbo na wale wa Viti Maalum vya Wanawake.

Hapa panataka mazingatio makubwa, kwani haiwezekani Mhe. Karume katika Serikali yake amteue Waziri kutoka Chama cha Upinzani kwa hoja ya kuwa almuradi Serikali aliyoiunda iwe na Mawaziri kutoka Pemba. Angelifanya hivyo angelikuwa amekikosea pakubwa Chama chake cha CCM. Na ingelikuwa kaikiuka hata katiba ya Chama chake. Wananchi wa Pemba hawana lazima ya kuteuliwa Uwaziri, kama walikuwa wanalitaka hilo basi wangaliandaa kwa maksudi Majimbo angalau matatu wakaipa CCM kwani walikuwa wanajua fika kuwa CCM lazima ingeshinda na kupata ridhaa ya kuunda Seikali. Sasa hapa wa kulaumiwa ni karume au Wapemba wajilaumu wenyewe kwa kutumia haki yao ya kidemokrasia bila ya kuzingatia.

Kwa kuwa Seif anatafuta pakushika hili nalo akalishika ooh! Karume katugawa wa Unguja na Pemba. Kuna mpasuko Zanzibar! Wapemba tunaonewa. Kwa bahati nzuri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete kaliona tatizo lililokuwepo Pemba. Kwani Pemba kuna kila aina ya vitendo vichafu, vilivyosababishwa na siasa. Migomo mwake ni kususiana, kuuziana bidhaa madukani na masokoni, talaka zilizotokana na misimamo ya kisiasa, kuhujumiana na kuumizana kwa sababu za kisiasa hata kufikia kuuana, kupakiana kinyesi katika majumba, kudharaulian, kususiana katika ibada, misiba, harusi na mambo mengi ya kijamii.

Kwa kuwa sasa yeye ndiye mwenye dhamana ya nchi, Kikwete alitamka wakati akilihutubia Bunge kwenye Uzinduzi wa Bunge kule Dodoma. Alisema Zaznibara liko tatizo la kisiasa na akaahidi kuwa atalishughulikia. Mimi kwa fikra zangu naamini matatizo niliyoyataja hapo juu ndiyo aliyo yaahidi kuyashughulikia Kikwete.

Kwa kuwa Seif Shariff alikuwa anatafuta la kushika. Aliona hili ndio la kukamata. Kauli hiyo ya Kikwete Seif Shariff na wenziwe kina Lipumba, wakaitia nakshi, wakairemba, wakaibirua kibirubiru na kuizushia mambo lukuki. Kuna mgogoro, kunampasuko Zanzibar, hakuna amani na utulivu Zanzibar, wananchi wamechoka na hali mbaya ya maisha na mambo mengine kem kem. Sasa mpigaji kaipata tutu aliyokuwa akiitafua, ataipiga hadi wa ng’ambo nao wasikie.

Chama cha CUF kilikaa kwa muda mrefu bila ya kiufanya mikutano ya hadhara. Baadhi ya wanachama wake walikuwa tayari wameanza kuvunjika moyo. Lakini mara tu, baada ya vinara wa CUF kuona kuwa wamepata kitu cha kuwaabia wafuasi wao mikutano ikaandaliwa haraka haraka kwani uongo wa kuambiwa wana CUF umepatikana.

Nakumbuka mkutano wa mwanzo ulifanyika katika viwanja vya Uwanja wa Demokrasia ambapo Juma Duni Haji alikuwa ndiye mzungumzaji mkubwa. Lililozungumzwa hapo ni ya kumzulia Kikwete kuwa amekiri kuwa Zanzibar kuna mpasuko na mgogoro wa kisiasa, na kuwa kaahidi kuushughulikia mpasuko na mgogoro huu.

Hapa wajinga wakainamishwa vichwa kwa kupakiwa uongo ambao chambilecho waswahili. “Uongo ambao hata hauna kizibo”. Hapo Rais Kikwete akapewa mud wa kushughulikia yaliyoitwa mgogoro wa Zanzibar. Kwanza alipewa muda wa miezi sita, mpaka itakapofika mwezi wa June 2006 mgogoro uwe umekwisha shughulikiwa.

Viongozi wa CUF walitoa muda huo kwani walijua kwa katika mwezi huo kutafanyika Mkutano Mkuu wa CCM ambao pamoja na kazi nyengine ulikuwa unakazi ya kumchaguwa Mwenyekiti mpya wa Chama Cha Mapinduzi. Na kwa mujibu wa utamaduni mwa CCM walijua wazi kuwa nafasi hiyo ilikuwa ya Jakaya Kikwete. Kauli ikawa kila wanapofanya mikutano yao ni kumshindikiza Kikwete kuwa aharakishe hatua zake za kuutatua mgoro wa kisiasa Zanzibar. Na kilasiku indhari ikitolewa kuwa pindipo asipotekeleza ahadi yake basi suala hilo litarudishwa kwa waliowaita wananchi.

Jambo la kushangaza katika suala hili, ni kuwa Rais Kikwete ikiwa ametamka na kuahidi kuutatua mgogoro wa kisiasa Zanzibar, si itakuwa yeye ameuona mgogoro wenyewe uliopo? Na ikiwa yeye Kikwete ameona Zanzibar upo mpasuko au mgogoro wa kisiasa, si yeye mwenyewe ndiye atakaetafuta njia na namna ya kushughulikia mgogoro huo?

Sasa iweje Seif Shariff na chama chake wawe tayari wameshafikia uamuzi wa njia za utatuzi wa mgogoro huo, kwa kudai kuwa ili mgogoro huo umalizike lazima Zanzibar iundwe Serikali ya Umoja was Kitaifa, ambayo itawashirikisha viongozi wa CCM na viongozi wa CUF. Hili nalo ni tatizo kubwa, kwani bado linaturudisha kulekule katika kuona kuwa Seif na wenzake wameubuni mgogoro ambao hauko ili kupata maslahi yao. Kwani tayari tumekwisha msikia yeye mwenyewe Seif akitamka katika mikutano ya hadhara na kwenye vyombo mbali mbali kuwa yeye yuko tayari kumsaidia Rais Karume au yuko tayari kufanya nae kazi katika Serikali ya Pamoja. Ili Karume aendelee kushika nafasi ya Urai na yeye Seif awe Waziri Kiongozi.

Kutokana na maelezo hayo, inonekana Seif Shariff kwa kipindi chote alichosubiri, tangu Mhe. Kikwete alipotamka kuwa atalishughulikia suala la Zanzibar, yeye alifahamu kwamba ile ilikuwa ni ahadi ya kutimizwa ndoto yake ya siku nyingi ya kuupata Uraisi wa Zanzibar. Na ata kama hakuupata Urais basi aambulie japo Uwaziri Kiongozi, Yaguju. Hilo haliwezekani! Kwani Rais Kikwete hawezi kulazimisha Zanzibar kuundwa Serikali ya Mseto, na kama atafanya hivyo atakuwa amekwenda kinyume na Katiba ya Chama Cha Mapinduzi.

Kwa kuwa Seif Shariff amekaa kusubiri matakwa yake kutoka kwa Kikwete kwa siku nyingi, na kwasababu yeye anauchu wa madaraka, muda ameuona mkubwa na siku zinapita bila kutimiziwa adhadi anayodhani kuwa ameahidiwa, ndiyo akaamua kuwa msanii kwa kuandaa mchezo wa kuigiza ambao hata mtoto mdogo anajua kuwa ule ulikuwa ni Usanii wa kisiasa tu.

Kitendo cha kuwakusanya wfuasi wake kwenye Ofisi CUF Mtendeni na kudai eti wamemzuia kuingia katika Ofisi hiyo ambayo ndio Makao Makuu ya Chama Chake lilikuwa ni la kutengenezwa. Ile ilikuwa chinja rero ya kubedua mdomo na kunoa mkono wa kulia kwa kushoto. Katika ulimwengu wa leo hata mtoto wa mwaka mmoja hashituki seuze mtu mzima mwenye akili timamu.

Seif Sharif aliandaa tukio lile ili ionekane kuwa kweli kuna wananchi Zanzibar waliochoka kusubiri kama yeye ili CCM na Rais Kikwete ashituke kwa kuona kuwa kama hakuharakisha kulishughulikia suala hili basi Zanzibar kutakuwa na maafa. Seif anajua fika kuwa yeye na Chama chake cha CUF wameshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 30, 2005,

Lakini kamatabia yake kuwa hakubali kushindwa. Na hali hii inatokana na Uchu wa madaraka alionao kiumbe huyu na anjua kuwa Zanzibar hakuna Uchaguzi mwengine mpaka 2010. Kwake yeye kusubiri hadi 2010 ni muda mrefu, hasa tukizingatia kuwa wanachama wake hwawezi kusubiri na kuvumilia kuiona Serikali ya Chama Cha Mapinduzi iko madarakani kwa muda wote huo. Katika kipindi hiki kabla ya kufikia wakati wa Uchaguzi Mkuu mwengine, Seif aonewe huruma angalau na yeye apatiwe nafasi katika Serikali angalau ajisikie.

Kwa kuwa Amani Abeid Karume amekubalika kitaifa na kimataifa, na jinsi Seif na Chama chake cha CUF wanavyomuona anavyofanikiwa katika kupata misaada ya kuijenga Zanzibar kwa kuikamilisha miradi mbali mbali ya maendeleo kwa kasi kubwa. Hili linawatia kiwewe kwani wanajua kuwa hata ikifika mwaka 2010 Serikali ya Amani itakuwa imetekeleza kwa kiasi kikubwa

Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu wa 2005 – 2010 ambayo ndiyo aliyoinadi Karume kwa wapiga kura wa Zanzibar na wakaamua kukipa ridhaa Chama Cha Mapinduzi kuongoza Dola. Au aseme wazi kwamba sasa Zanzibar upinzani basi yeye amechoka? Sasa Seif na wafuasi wake watuambie. Hiyo Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakuja kutekeleza Sera gani? Wakati Sera za CCM na za CUF hazifanani wala hazikubaliani.

Tuchukue mambo mawili ya msingi wa Sera za CCM na jinsi zinavyotofautiana na CUF. Kwnza katika suaala la Uhuru wa Zanzibar CCM inaami kuwa Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 ndiyo yaliyomkomboa Mzanzibar. Wakati CUF inaamini Uhuru wa Disemba 10, 1963 Uhuru ambao Mwingereza alimkabidhi Sultani wa Kimanga. Na la pili ni juu ya Sera ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, CUF inataka uwe wa Serikali tatu wakati CCM sera yake ni Muungano wa Serikali mbili. Je mseto wa mchele na mawe unalike? Au Seif anataka kutuletea vurugu ndani ya Zanzibar.

Jambo hili linamvunja moyo Seif, ndiyo maana sasa anatafuta kila aina ya mbinu ili na yeye awemo Serikalini ili apate nafasi ya kuivuruga Serikali isifanikiwe kutekeleza Ilani ya CCM. Na hapa napenda kuchukua nafasi hii, kuwambia viongozi wengine wa vyama vya upinzani kuwa wasicheze ngoma wasioijua. Lengo la Seif sio Upinzani, hebu wakumbuke matokeo ya Uchaguzi mdogo wa Majimbo 17 ya Pemba. Baada ya kuenguliwa Wagombea wa CUF mbona hakutoa amri kuwa kura kipewe chama chengine chochote cha upinzani! Badala yake kasema kura wapewe Maruhani. Msikaange mbuyu kuwachia vibogoyo kutafuna.

Kwa hivyo ninachoweza kusema hapa kuwa Zanzibar hakuna mgogoro wala mpasuko, isipokuwa ni mgogoro wa kutengenezwa na Seif Sharif na Chama chake CUF ili kukidhi maslahi yao binafsi na wala si kwa maslahi ya Wazanzibar. Wazanzibari walikwishakutoa maamuzi yao tangu Otoba 30, 2005 kwa kukipa ridhaa Chama Cha Mapinduzi kuongoza Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano hadi kufika 2010. Seif Shariff kama halikubali hilo basi sio mwana demokrasia. Kwani kanuni ya demokrasi inasema maamuzi ya wengi ndiyo maamuzi ya wote. Hata kwa sisi waumini wa Dini ya Kiislamu tunaamini kuwa, penye maamuzi ya wengi basi na mkono wa Mungu upo!

No comments: